Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Jalala ametoa nasaha hizo jana, katika khutuba ya Swala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti wa Ghadir, ambapo alieleza kuwa; Waislamu kukutana katika miezi hii ya Rabiul Awwal na thaani, kwa ajili ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni jambo jema na lenye umuhimu mkubwa katika kuimarisha mapenzi juu ya Mtume na kumkumbuka Mwenyezi Mungu.
Katika mwanzo wa khutuba yake, Sheikh Jalala alisoma aya mbili za Qur’ani Tukufu kutoka katika Suratul Aal Imran, zinazozungumzia alama za uwezo wa Mwenyezi Mungu katika uumbaji wa mbingu na ardhi, mabadiliko ya usiku na mchana, pamoja na sifa za waumini wanaomdhukuru Mwenyezi Mungu katika hali mbalimbali za maisha yao.
Mwenyezi Mungu anasema:
إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِأُولِي الْأَلْبَابِ
“Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana, zimo ishara kwa wenye akili.”
(Suratul Aal Imran: 190).
Pia Mwenyezi Mungu anasema:
الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ
“Wale ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima, wameketi na wakiwa wamelala kwa ubavu, na hutafakari kuhusu kuumbwa kwa mbingu na ardhi, wakisema: ‘Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto.’”
(Suratul Aal Imran: 191).
Akizifafanua aya hizo, Sheikh Jalala alisema kuwa; katika ukanda wa Afrika Mashariki, Waislamu wamekuwa wakikutana mara kwa mara katika miezi hii ya Rabiul Awwal na thaani, ili kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), akibainisha kuwa mikusanyiko hiyo ni fursa muhimu ya kuhuisha mapenzi kwa Mtume na kuimarisha dhikri katika jamii.
Alisisitiza kuwa; miongoni mwa matendo yenye fadhila kubwa ni kumswalia Mtume Muhammad (s.a.w.w), kwani kumtaja Mtume na kumtakia rehema na amani ni sehemu ya ibada zinazomkumbusha mwanadamu Mwenyezi Mungu na kumkuribisha zaidi Kwake.
Aidha, alisema kuwa aya hizo zinatufundisha umuhimu wa kumdhukuru Mwenyezi Mungu katika hali zote, iwe mtu amesimama, ameketi au amelala, sambamba na kutafakari juu ya uumbaji Wake. Kwa mujibu wa maelezo yake, muumini anapaswa kuifanya dhikri kuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku badala ya kuifanya kuwa ibada inayofanyika katika nyakati maalumu pekee.
Wosia wa Mtume (s.a.w.w) kwa Abu Dharr kuhusu madhambi na toba
Katika kuendeleza khutuba yake, Sheikh Jalala alirejelea baadhi ya vipengele vya wosia wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kwa Swahaba wake Abu Dharr al-Ghifari, vinavyofafanua namna mwanadamu anavyopaswa kuzingatia matendo yake, kuogopa madhambi na kutumaini rehema ya Mwenyezi Mungu.
Katika riwaya ya kwanza, Mtume (s.a.w.w) anamwambia Abu Dharr:
يَا أَبَا ذَرٍّ، إِنَّ الْعَبْدَ لَيُعْرَضُ عَلَيْهِ ذُنُوبُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، فَيَذْكُرُ ذُنُوبَهُ، فَيَقُولُ: أَمَا إِنِّي كُنْتُ خَائِفًا مُشْفِقًا، فَيُغْفَرُ لَهُ.
“Ewe Abu Dharr! Hakika madhambi ya mja yatawekwa mbele yake Siku ya Kiyama, naye atayakumbuka madhambi yake na kusema: ‘Hakika nilikuwa nikihofu na kuogopa matokeo yake.’ Basi atasamehewa.”
Akifafanua mafunzo ya riwaya hiyo, Sheikh Jalala alisema kuwa; baadhi ya watu hujikuta wameanguka katika makosa na madhambi, lakini baadaye hutambua uzito wa makosa yao, huingiwa na hofu na kujuta kwa yale waliyoyatenda, hali hiyo ya kujutia na kuogopa matokeo ya madhambi humfanya mwanadamu arejee kwa Mwenyezi Mungu na kutafuta msamaha wake, akibainisha kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa rehema na msamaha kwa waja wake wanaorejea kwake kwa unyenyekevu na majuto ya kweli na ndio maa Humsamehe mja wake huyu.
Katika kipengele kingine cha wosia huo, Mtume Muhammad (s.a.w.w) anamwambia Abu Dharr kuhusu hatari ya kuyadharau madhambi madogo na kujiona salama kutokana na matendo mema ambayo mtu ameyafanya.
Mtume (s.a.w.w) anasema:
يَا أَبَا ذَرٍّ، إِنَّ الرَّجُلَ لَيَعْمَلُ الْحَسَنَةَ فَيَتَّكِلُ عَلَيْهَا، وَيَعْمَلُ الْمُحَقَّرَاتِ حَتَّى يَأْتِيَ اللَّهَ وَهُوَ عَلَيْهِ غَضْبَانُ، وَإِنَّ الرَّجُلَ لَيَعْمَلُ السَّيِّئَةَ فَيَفْرَقُ مِنْهَا، فَيَأْتِي آمِنًا يَوْمَ الْقِيَامَةِ.
“Ewe Abu Dharr! Hakika mtu anaweza kufanya tendo jema kisha akalitegemea na kujiona ametosheka nalo, huku akiendelea kufanya madhambi madogo anayoyadharau, mpaka anapokutana na Mwenyezi Mungu hali ya kuwa Amemkasirikia. Na hakika mtu mwingine anaweza kufanya tendo baya, kisha akaingiwa na hofu kwa sababu yake, na hivyo akaja Siku ya Kiyama akiwa katika hali ya usalama.”
Akifafanua riwaya hiyo, Sheikh Jalala alisisitiza kuwa: Mwanadamu anapaswa kujiepusha na madhambi yote, yakiwemo yale anayoyaona kuwa madogo au yasiyo na athari kubwa. Alionya kuwa kuyadharau makosa kunaweza kumfanya mtu aendelee kuyatenda bila kujali matokeo yake mbele ya Mwenyezi Mungu.
Aidha, aliwahimiza waumini kuharakisha kutubia wanapoteleza na kufanya dhambi, badala ya kuchelewesha toba au kujidanganya kwa kutegemea matendo mema waliyoyafanya hapo awali. Alieleza kuwa mtu hapaswi kujiona salama kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa sababu tu ametenda baadhi ya mema, bali anatakiwa kuendelea kujitathmini, kujirekebisha na kuomba msamaha.
Katika kuhitimisha maelezo yake kuhusu kipengele hicho, Sheikh Jalala alisisitiza kuwa hofu ya Mwenyezi Mungu na kujutia makosa ni mambo yanayopaswa kumwelekeza mwanadamu katika toba na kujiepusha na madhambi, huku akidumisha matumaini katika rehema ya Mola wake.
Toba ya kweli inaweza kuwa sababu ya wokovu wa mwanadamu
Katika mwendelezo wa khutuba yake, Sheikh Jalala alirejelea kipengele kingine cha wosia wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kwa Abu Dharr, kinachofafanua namna dhambi inavyoweza kuwa sababu ya mwanadamu kujifunza, kutubu na kurejea kwa Mwenyezi Mungu, mpaka toba hiyo ikawa sababu ya kupata msamaha Wake.
Mtume (s.a.w.w) anasema:
يَا أَبَا ذَرٍّ، إِنَّ الْعَبْدَ لَيُذْنِبُ الذَّنْبَ فَيَدْخُلُ بِهِ الْجَنَّةَ، فَقُلْتُ: وَكَيْفَ ذَلِكَ بِأَبِي أَنْتَ وَأُمِّي يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ قَالَ: يَكُونُ ذَلِكَ الذَّنْبُ نُصْبَ عَيْنَيْهِ، تَائِبًا مِنْهُ، فَارًّا إِلَى اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ حَتَّى يَدْخُلَ الْجَنَّةَ.
“Ewe Abu Dharr! Hakika mja anaweza kutenda dhambi, kisha akaingia Peponi kwa sababu yake.” Nikasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, baba yangu na mama yangu wawe fidia yako! Hilo linawezekanaje?” Akasema: “Dhambi hiyo hubaki mbele ya macho yake; huwa ametubu kutokana nayo na anamkimbilia Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mwenye Utukufu, mpaka anaingia Peponi.”
Mafunzo yanayopatikana katika riwaya hii ni kwamba mwanadamu anapofanya dhambi hapaswi kuendelea kuishi katika hali ya kupuuzia kosa lake, bali anapaswa kulikumbuka kwa namna inayomchochea kujuta, kutubu kwa dhati na kumrudia Mwenyezi Mungu.
Kwa msingi huo, kosa linaweza kuwa sababu ya mtu kujirekebisha na kuimarisha uhusiano wake na Mola wake, ikiwa litampelekea katika toba ya kweli na kuacha maasi. Hata hivyo, jambo hilo halimaanishi kuwa dhambi yenyewe ni tendo jema, bali kinachoweza kuwa sababu ya wokovu ni kurejea kwa Mwenyezi Mungu kwa toba ya kweli na kuendelea kujiepusha na makosa.
Kupitia mafunzo hayo ya Qur’ani Tukufu na wosia wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kwa Abu Dharr al-Ghifari, waumini wamekumbushwa umuhimu wa kumdhukuru Mwenyezi Mungu, kumswalia Mtume Wake, kutokudharau madhambi na kuharakisha kutubia pindi wanapokosea, huku wakiendelea kutumaini rehema na msamaha wa Mwenyezi Mungu.
Maoni yako